Wednesday, August 3, 2016

STORI KUHUSU MICHEZO; TAARIFA KUHUSU MOHAMED DEWJ "MO" NA TIMU YA SIMBA SC

MOHAMED DEWJ"MO" MFANYABIASHARA TAJIRI TANZANIA
 
MFANYABIASHARA Mohamed Dewji ‘Mo’ jana alikabidhi mfano wa hundi ya Sh milioni 100 kwa uongozi wa Simba kwa ajili ya kusaidia usajili.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mo alisema ametoa fedha hizo kama mchango wake katika usajili wa Ligi Kuu unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki hii.
Akipokea hundi hiyo Rais wa Simba, Evans Aveva alimshukuru Mo kwa msaada huo na kwamba fedha hizo zitasaidia kumsajili mchezaji raia wa Ivory Coast, Fredrick Blagnon ambaye kwa mujibu wa Aveva anahitaji Sh milioni 110.
“Fedha hizi zitasaidia kufanya usajili wa Muivory Coast, tulihitaji Sh milioni 420 ili kukamilisha sehemu ya usajili iliyobaki hivyo bado tunahitaji Sh milioni 320 kukamilisha usajili,” alisema ingawa hakusema bajeti nzima ya usajili ya klabu hiyo ni kiasi gani.
Mo Dewji aliahidi kuchangia usajili wa Simba iwapo wanachama wa klabu hiyo watakubali mabadiliko kutoka kwenye mfumo wa klabu kumilikiwa na wanahisa.
Na Mkutano wa mwishoni mwa wiki iliyopita uliofanyika Bwalo la Polisi Osterbay wanachama wa Simba walikubali mabadiliko na kuingia kwenye mchakato wa kuuza hisa.
Mo alitoa sharti hilo sambamba na ofa ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh bilioni 20 iwapo mabadiliko yatapitishwa. Akizungumzia tuhuma za kukwamisha mpango wa Mo, Aveva alisema hazina ukweli wowote na kwamba hatarajii kufanya hivyo.
“Si kweli nakwamisha mabadiliko, niliunda kamati ya kufanya mchakato wa mabadiliko, ningekuwa siafiki nisingeunda kamati na nisingeunga mkono mabadiliko, mimi ni muumini wa mabadiliko na nitahakikisha nayasimamia,”alisema Aveva.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Mjini na mwanachama wa Simba, Kabwe Zitto ameshauri kwenye muundo wa umiliki, mtu mmoja asiwe na hisa zaidi ya asilimia 40 hiyo itasaidia kumpunguzia madaraka ya maamuzi moja kwa moja.
“Kuna hatari ukimpa mtu mmoja uwezo wa kufanya maamuzi peke yake lazima kumfanya ashawishi japo kwa asilimia 11 ya wenye hisa ili kuboresha maamuzi”.

No comments:

Post a Comment