Wednesday, August 3, 2016

KUTOKA MOROGORO TANZANIA;Serikali kupitia upya kilimo cha mkataba

WAZIRI MKUU WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA
 
story by JULIE KAVISHE-JOURNALIST MACHAS BLOG...

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaangalia upya matumizi ya mfumo wa kilimo cha mkataba ambao umewaingizia wakulima hasara kubwa kutokana na kulazimika kuuza mazao kwa bei ndogo.
Majaliwa alisema hayo juzi alipokuwa akifungua Maonesho ya Wakulima ya Nanenane, Kanda ya Mashariki kwenye Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mjini hapa. Alisema mfumo huo wa kilimo cha mkataba umechangia kwa kiwango kikubwa kudidimiza kilimo cha pamba hasa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Alisema kilimo cha mkataba pamoja na uzuri wake wakulima kukopeshwa pembejeo za kilimo, lakini kilimo cha aina hiyo kimekuwa kikiwakandamiza na kuwanyonya wakulima juu ya mazao yao kwa kutokuwa huru kuuza bei inayowaletea tija, badala yake walioingia mkataba nao kuwapangia bei ndogo ya kununua mazao yao bila kujali ushindani katika soko.
“Kwa sasa serikali inaangalia upya matumizi ya mfumo wa kilimo cha mkataba kimeonekana kimewaingizia wakulima hasara kubwa kutokana na kuwakandamiza na kuwalazimisha wauze mazao yao bei ndogo," alisema.
Alisema wakati serikali ikiendelea kuboresha mfumo huo, aliagiza halmashauri zote kuweka mikakati ya kuwawezesha wakulima kuhifadhi na kuuza mazao yao kwa mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amerejea kauli yake ya kupiga marufuku ufungashaji wa mazao kwa kuweka lumbesa kwa kuwa ni moja ya njia ya kuwanyonya wakulima ambao wanatumia nguvu nyingi kuliko faida wanayoipata pale wanapouza mazao yake.
Pia Majaliwa aliwasihi wafugaji wasikubali kuuza mifugo yao kwa kuangalia bali kwa kutumia mizani, hivyo kuzitaka halmashauri zote kuhakikisha minada yote inakuwa na mizani za kupimia mifugo, waweke maeneo ya bei kulingana na uzito na wanunuzi watakaokaidi agizo hilo washughulikiwe kisheria.

#MACHAS OFFICIAL SITE

No comments:

Post a Comment