Friday, December 23, 2016
MCHAGGA NA ASILI YAKE: HIZI NI SABABU CHACHE ZA KWA NINI WACHAGGA HUPENDELEA KWENDA KWAO KILA MWISHO WA MWAKA(CHRISTMAS & NEW-YEAR)>>>
ANAANDIKA HENRY KILEWO>>>>>
Nimeamua kuandika kipande cha waraka huu kutokana na kuwepo kwa dhana nyingi potofu juu ya wachagga kwenda kwao kipindi cha mwisho wa mwaka, maarufu kama "kwenda kuhesabiwa".
Je ni kweli wachagga huenda kuhesabiwa? Jibu ni Hapana.. si kweli. Wachagga hawaendi kuhesabiwa.
SWALI; Sasa kama hawaendi kuhesabiwa neno "kuhesabiwa" limetoka wapi na kwanini litumike kwao tu sio kwa Wasukuma, Wamasai, Wayao au Wamakonde?
JIBU; Neno "kuhesabiwa" limetoholewa kutoka neno la Kiebrania "מִפקָד אוֹכלוּסִין" linalomaanisha Wana wa Israel kurudi kwao kwa ajili ya kuhesabiwa.
Mara nyingi Waisrael walikua wanarudi kipindi cha mwisho wa mwaka wa Kiyahudi ktk mwezi uitwao "Adar Beit" ambao kwa mujibu wa Kalenda ya Kiyahudi huo ndio mwezi wa mwisho wa mwaka. Na hukaa huko hadi mwezi wa kwanza wa mwaka ambao kwa kiyahudi huitwa "Nissan".
Utamaduni huu ulitumika ktk Israel ya zamani (Ancient Jews) japo kwa sasa haupo tena. Katika kipindi hiki Waisrael walikua wakikutana nyumbani na kupanga mipango ya maendeleo pamoja na kuhesabiwa ili kujua idadi yao kutokana na kutawanyika katika mataifa mengi duniani.
Tangu enzi za Musa miaka zaidi ya 4,000 kabla ya Kristo; Waisrael walikua na utamaduni wa kurudi kwao kuhesabiwa.
Katika kitabu cha 1 Nyakati 23:2-3 Biblia inasema "Akawakusanya wakuu wote wa Israeli, pamoja na makuhani na Walawi. Nao wakahesabiwa Walawi wenye miaka thelathini na zaidi; na jumla yao kwa vichwa, mtu kwa mtu, ikapata thelathini na nane elfu."
Huu ni udhibitisho wa kuhesabiwa kwa Wana wa Israel zamani hizo. Lakini pia kitabu cha Hesabu 3:14-15 kinasema "Kisha Bwana akanena na Musa huko katika bara ya Sinai, na kumwambia, Uwahesabu wana wa Lawi kwa kuandama nyumba za baba zao na jamaa zao; kila mtu mume tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi utawahesabu."
Maandiko yanayoeleza juu ya kuhesabiwa kwa wana wa Israel ni mengi na unaweza kuyasoma baadae ktk (Kutoka 12:37, Waamuzi 20:14, 1 Samweli 11:8, Ezra 2:64).
Kwa hiyo kuhesabiwa ni agizo la Mungu na utamaduni huu wa wana wa Israel kurudi kwao kwenda kuhesabiwa ni utamaduni uliokua maagizo ya Mungu mwenyewe (Jehovah).
Sasa je ikiwa Wachagga hawaendi kuhesabiwa iweje wafananishwe na WaIsrael?
Sababu mbili hufanya wachagga kufananishwa na utamaduni huu wa Israel wa kuhesabiwa.
SABABU YA KWANZA ni kitendo cha wachagga kurudi kwao mwishoni mwa mwaka (December) na kukaa huko hadi mwanzoni mwa mwaka mpya (January). Ikumbukwe wana wa Israel nao huenda kwao mwishoni mwa mwaka wa Kiyahudi (Adar Beit) na kurejea mwanzoni mwa mwaka mpya (Nissan). Ufanano huu wa majira hufanya wachagga nao waonekane kuwa wanaenda "kuhesabiwa" kama waIsrael.
SABABU YA PILI ni mtawanyiko wa jamii hizi mbili. Wana wa Israel wametawanyika ktk mataifa mbalimbali duniani. Kutokana na ufinyu wa nchi yao wamejikuta wakisambaa nchi mbalimbali ambapo wanaishi na kufanya kazi huko. Wengine ni wahandisi, madaktari, majemadari wa vita etc. Wana wa Israel wametawanyika mataifa yote ya Ulaya, America na baadhi ya nchi za Asia na Afrika. Pamoja na kutawanyika huku lakini mwisho wa mwaka hukumbuka kurudi kwao.
Kwa upande wa wachagga nao wametawanyika sana ktk mikoa mbalimbali nchini. Mtawanyiko wao unafananishwa na ule wa wana wa Israel kwa sababu mbili. Kwanza eneo lao la makazi (Kilimanjaro) ni dogo na haliwatoshi, sawa na Israel ilivyo ndogo na isivyotosha watu wake. Pili ni "nature" ya mtawanyiko wao. Wachagga kama Waisrael wametawanyika sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya nchi.
Hakuna mkoa au Wilaya yeyote unaweza kwenda nchini ukamkosa Mchagga. Wametapakaa kila kona ya nchi wakifanya shughuli mbalimbali hususani biashara. Mtu mmoja aliwahi kutania kuwa "ukienda eneo la nchi hii ukakosa Mchagga ondoka haraka maana hapafai kuishi".. Hii ina maanisha Wachagga wanaweza kuishi ktk mazingira yoyote na hali yoyote.
Mtawanyiko wa Wachagga ktk maeneo mbalimbali ya nchi hufananishwa na mtawanyiko wa Waisrael ktk maeneo mbalimbali ya dunia, na hivyo basi kitendo cha Wachagga kurudi kwao mwishoni mwa mwaka hufananishwa na kitendo cha Waisrael kurudi kwao mwishoni mwa mwaka wa kalenda ya kiyahudi. Tofauti ni kuwa Waisrael huenda kuhesabiwa lakini Wachagga hawaendi kuhesabiwa.
KAMA WACHAGGA HAWAHESABIWI, WANAENDA KUFANYA NINI?
Pengine hili ndio swali la msingi ambalo wengi wanajiuliza. Ikiwa wachagga hawaendi kuhesabiwa kama ilivyo kwa waisrael, Je wanaenda kufanya nini?
Ukweli ni kwamba Wachagga wanakwenda kwao kwa sababu mbalimbali. Leo nitaainisha kwa uchache sababu 10 zinazorudisha wachagga kwao kila mwisho wa mwaka.
Zipo nyingi zaidi ila kwa kifupi ni kama ifuatavyo;
1. Kuna wanaokwenda kwao kwa ajili ya kuonana na familia zao na kuwaona wapendwa wao na kujumuika nao kwa ajili ya kufurahia sikukuu za mwisho wa Mwaka huhusani "Krismasi" na "Mwaka mpya".
Kwa mfano wazazi wako (baba na mama) au ndugu zako wengine (babu, bibi, kaka, dada, shangazi, wajomba etc) hujawaona kwa kipindi cha mwaka mzima. Mmekuwa mkiwasiliana tu kwa simu. Hivyo basi December huwa ni kipindi kizuri cha kurudi nyumbani na kuwaona na kuwajulia hali.
2. Pia kipindi hiki hutumika kupanga mipango ya maendeleo ya familia kama vile kujenga. Kwa kuwa watoto wote wa familia hukutana kipindi hiki basi huweka mipango ya maendeleo kwa familia yao. Wanaweza kupanga kujenga nyumba kwa ajili ya wazazi wao ambao ni wazee, kuweka umeme, maji etc.
Uchaggani ni mojawapo ya maeneo nchini ambako kuna nyumba nyingi za kisasa vijijini na ni mkoa uliofanikiwa kupiga vita nyumba ya Nyasi tangu mwaka 1996.
Ni jambo la Kawaida kukutana na maghorofa ya kisasa kule "Machame Uswaa, Kibosho Kirima, au Mamba Komakundi".. au ukipita "Uru Mawela, Rombo Mamsera au Kilema Poffo" nyumba zote unazokutana nazo ni self-contzined za kisasa, lakini wanaishi wazee. Watoto wao wapo Shinyanga, Dar, Kigoma, Mwanza etc wanatafuta maisha. Mipango hiyo ya kujenga na kuhudumia wazazi hupangwa msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
3. Msimu huu wa sikukuu hutumika kupatanisha ndugu, jamaa au marafiki waliokosana. Wazee huitwa na kuzungumza na pande zote mbili kisha kuwapatanisha. Mkikubali kuelewana basi huchinjwa mbuzi kama ishara ya furaha ambapo jamii yote hujumuika kwa kula na kunywa.
4. Kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ndio kipindi kizuri ambacho vijana hukitumia kutambulisha wachumba zao nyumbani. Unaweza kuwa unaishi Dar na umepata mchumba wa Morogoro. Lakini ndugu zako wametawanyika. Wengine wapo Tabora, wengine Mwanza, wengine Mbeya. Huwezi kupita na mchumba wako kote huko kumtambulisha. Kwahiyo "option" nzuri ni kusubiri msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo ndugu zako wote watakuwepo nyumbani ndipo umpeleke mchumba wako kumtambulisha, na kupanga mipango ya ndoa.
5. Kuwaleta watoto wafahamu ndugu zao na wafahamike nyumbani. Unaweza kuwa unaishi Dar na familia lakini ndugu zako wanaishi na familia zao maeneo mengine ya nchi, watoto wenu hawafahamiani maana hawajawahi kuonana. Hivyo mkikutana nyumbani msimu wa sikukuu ni kipindi kizuri cha watoto wenu kufahamiana na kufahamu asili yao.
Pia ikiwa umejaliwa mtoto ukiwa huko unakofanyia shughuli zako lakini wazazi wako hawajamuona mjukuu wao, hiki ni kipindi kizuri cha kuwapelekea wazazi wako mjukuu wao wamuone na kumpa Baraka.
6. Kushiriki shughuli za kijamii (charity work). Wachagga wengi ni waumini wazuri sana wa dini iwe ukristo au uislamu. Hivyo kipindi cha msimu wa sikukuu hutenga muda wa kutembelea wagonjwa, Yatima na Wasiojiweza na kuwapa misaada mbalimbali. Kwa wale Wakristo huita "sadaka ya Epifania".
7. Kipindi hiki hutumika pia kufanya usafi na kurekebisha maeneo waliyopumzika wapendwa wetu (makaburi). Wachagga kama ilivyo binadamu wengine hutenga maeneo maalumu ya kuzikia ndugu zao; na mara nyingi kila familia ina eneo lake.
Kwa hiyo ikiwa kuna ndugu amefariki na akazikwa basi msimu huu huwa ni kipindi kizuri cha kujengea makaburi kama kumbukumbu ya sehemu walipopumzika wenzetu.
Bahati mbaya wapo watu wanaohusisha utamaduni huu na matambiko. Kwanza ieleweke kujengea makaburi si dhambi na si matambiko. Hata Yakobo alipofia kule Misri alipoenda kwa mwanae Yusufu alizikwa kwenye Kaburi lililojengewa (Matendo 7:15-16). Hivyo basi ni vizuri ikaeleweka kuwa kujengea makaburi si dhambi.
Na mara nyingi uchaggani kabla ya kujengea Kaburi kiongozi wa dini huitwa na kufanya sala, kabla ya shughuli ya ujenzi haijaanza. Kwahiyo hakuna nafasi ya matambiko.
Ikiwa kuna mchagga anafanya matambiko wakati wa kujengea makaburi ichukuliwe kuwa ni tabia ya mtu binafsi na isihuhishwe wachagga wote. Kwani wapo watu wa makabila mengine hufanya matambiko pia lakini huwezi kusema jamii yote hutambika
8. Msimu huu wa sikukuu ni kipindi kizuri ambacho wachagga hukitumia kupanga na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii yao kama vile mashule, hospitali, Maji, barabara n.k
Kwa mfano zipo barabara nyingi ambazo zimejengwa kwa nguvu ya wananchi wenyewe kwa kuamua kujichangisha bila kusubiri serikali ifanye. Barabara ya Uru Kusini ni mojawapo. Mipango hii hupangwa msimu huu wa sikukuu.
9. Msimu huu hutumika kwa ajili ya mapumziko ya familia baada ya mahangaiko ya mwaka mzima. Ni wakati wa familia kutulia pamoja kutafakari mipango ya mwaka uliopita na kuweka mipango mipya ya mwaka unaofuata.
Ndugu na jamaa hukutana pamoja na kufurahia sikukuu za "Krismasi" na "mwaka mpya" kwa kula na kunywa hasa vyakula vya asili kama "kisusio, faya, supu ya mbuzi iliyopikwa kiasili kwa kuchanganywa na majani aina ya "mahombo" na vyakula vingine bila kusahau kinywaji aina ya mbege.
10. Kipindi hiki hutumiwa kujenga na kukarabati nyumba za ibada. Ni wazi kuwa Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo ambayo kuna nyumba nzuri na za kisasa za Ibada.
Kanisa kubwa na la kisasa kama la KKKT Old-Moshi Rau, au La RC Kristu Mfalme, Au TAG Kilimanjaro Revival, au Msikiti wa kisasa kama wa Riadha, ni nadra kuvipata mahali pengine. Au Kanisa la kale kama la KKKT Old-Moshi Kidia lililojengwa mwaka 1843 utalipata wapi kwingine?
Mipango ya ujenzi wa nyumba hizi za ibada za kisasa na kukarabati zile za zamani hufanywa msimu huu wa sikukuu.
Pia wachagga wengi hupenda kwenda kwao kwa kuwa ibada zote ktk msimu huu huongozwa kwa kichagga. Yani kuanzia usomaji wa misa, mahubiri hadi nyimbo huimbwa kwa kichagga, wakati huo nyumba za ibada zimepambwa kwa mapambo ya asili kama "Makurera, makangachi, migomba imechimbiwa vichumini (njia za kwenda nyumbani)" etc.
Hii huongeza nakshi na kufanya mtu ajisikie kupungukiwa kitu ikiwa hatakuwepo Nyumbani msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
NB: Utamaduni huu wa Wachagga ni mzuri sana, na kuna mengi jamii nyingine zinaweza kujifunza kupitia Wachagga kama ambavyo wachagga wanaweza kujifunza kupitia jamii nyingine.
Tuukatae uzungu, tujivunie vya kwetu. Jivunie usukuma wako, jivunie Usambaa wako, jivunie Unyakyusa wako, jivunie Umasai wako, Jivunie Ungoni wako, najivunia Uchagga wangu. SI KOSA kujivunia kabila lako lakini NI KOSA kutumia kabila lako kumbagua mtu wa kabila jingine......
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment