Wednesday, September 7, 2016

HATIMAYE MTATIRO ‘AMCHANA’ PROF. LIPUMBA, AMUITA NI JEMEDARI ALIYEKIMBIA VITA >>>>>>>

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amesema aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba amekiacha chama kwenye wakati mgumu baada ya kujiuzulu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Agosti, mwaka jana, Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo na kukabidhi barua kwa uongozi baada ya kushauriana kwa kipindi kirefu na viongozi na wazee wa chama hicho, akisema nafsi yake inamsuta kwa kuwa walikiuka malengo ya Ukawa.
Hata hivyo, hivi karibuni Profesa Lipumba aliandika barua ya kutengua uamuzi wa kujiuzulu na uchaguzi ulipoitishwa ili kujaza nafasi hiyo hakuchukua fomu ya kugombea.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mtatiro amesema Profesa Lipumba amekitelekeza chama kikiwa katikati ya uwanja wa mapambano.
Mtatiro aliyeteuliwa hivi karibuni na Baraza Kuu la CUF kuongoza kamati ya uongozi wa chama hicho baada ya kuvunjika kwa mkutano mkuu ulioitishwa kuziba nafasi ya mwenyekiti, amesema walijaribu kila mbinu kumshauri Profesa Lipumba asijiuzulu bila mafanikio.
“Tukamuuliza kama ni kujiuzulu kwa nini usifanye baada ya uchaguzi? Kwa sababu wewe ndiye jemedari wa vita, wewe ndiye uliyeleta mabadiliko, wewe ndiye mwenyekiti wa Ukawa, sasa leo vita ndiyo inaanza umeshapeleka askari mstari wa mbele halafu unarudi nyumbani. Askari kule mstari wa mbele unamwachia nani?” alisema  na kuongeza:
“Kwa hiyo Profesa Lipumba aliondoka na alituacha katika wakati mgumu sana. Kwa sababu sasa unamwachia chama Shaweji Mketo (Mkurugenzi wa Uchaguzi- CUF) aende kugawana majimbo na kina Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), yule ni kijana, wale ni wazee…”
Alisema Profesa Lipumba alipoondoka CUF, heshima ya chama ilishuka kwa sababu hakukuwa na mtu mwenye uwezo wa kujadiliana na viongozi wengine wa Ukawa na pia ilipoteza majimbo waliyoyatarajia kuyapata katika uchaguzi.
Aliongeza kuwa CUF ingeweza kupata zaidi ya majimbo 25 kama Profesa Lipumba angekuwapo, lakini yalichukuliwa na vyama vingine.
“Kwa hiyo kupata majimbo 10 ilikuwa ni kwa sababu ya kuondoka kwa Lipumba. Haya jemedari amekimbia vita, amesusa kwa sababu ya Ukawa. Lakini tulitarajia aende kunadi wagombea wake wa CUF, maana yeye ni mwanachama,” amesema Mtatiro.
 

No comments:

Post a Comment