Monday, June 27, 2016

Mambo 17 Ya Kufanya Ili Kupunguza Msongo Wa Mawazo (Stress) Na Kuwa Na Furaha Zaidi.


Maisha yamebadilika. Dunia inakwenda kwa kasi kuliko kawaida. Kila mtu yupo “bize”. Muda umekuwa “adimu”. Kuna matukio mengi ambayo hayakuwepo miaka ya nyuma. Kwa mfano, leo hii kuna maradhi mengi kuliko miongo mitatu ya nyuma. Ugaidi umepamba moto ulimwenguni. Hofu imetawala.Umasikini umezidi.
Utu umekuwa kitu adimu. Gharama za maisha zimepanda. Kupata chochote sharti uingie ndani ya mfuko. Matokeo yake ni wengi kukumbwa na msongo wa mambo au mawazo (stress) kwa kutumia lugha ya kuazima.
Sote, katika wakati huu au mwingine, hujikuta au kupatwa na kitu kinachoitwa msongo wa mawazo(stress). Kila kitu unakiona kinakwenda kombo. Huna tena raha au amani. Kazini unapaona kama kituo cha polisi. Nyumbani unapaona kama jela.Kulala huwezi. Kula huwezi. Huoni sababu ya kuendelea kuishi. Unajihisi uliyeshindwa. Ufanyeje unapokumbwa na hali hiyo?
Ingawa sio kila aina ya msongo wa mawazo ni kitu kibaya, mara nyingi stress sio kitu kizuri kiafya na hata kiutendaji. Ingawa tunashauriwa “maumivu yakizidi muone daktari”, yapo mambo kadhaa ambayo unaweza kuyafanya kabla ya kumuona daktari. Kuna hatua unazoweza kuchukua. Hizi hapa chini ni ambazo mimi binafsi huzitumia pindi maji yanapoonekana kuzidi unga. Badala ya ugali,unatokea uji. Naamini na wewe unazo mbinu kadhaa. Ningependa kuzijua. Tafadhali niandikie kupitia kisanduku cha maoni.
  1. Kubaliana na ukweli kwamba kuna mambo huwezi kuyabadili. Ubinadamu una mipaka. Kuna ambayo tunaweza kuyafanya au kuyabadilisha. Litizame jambo linalokupa msongo wa mawazo kwa makini. Je,lipo ndani ya uwezo wako? Kama halipo, usihangaike. Muachie Mungu. Badala yake pambana kubadili yale ambayo yapo ndani ya uwezo wako. Kuna msemo wa kiingereza huwa naupenda; Sometimes the best thing you can do is not think, not wonder,not imagine,not obsess.Just breathe, and have faith that everything will work out for the best.
  1. Kubali Mabadiliko– Dunia ya leo inabadilika kila siku na kwa kasi sana. Kuna mambo ambayo yanaweza kukukwaza. Yapo mambo ambayo yanaenda kinyume kabisa na imani zako. Kubaliana na hali halisi. Sio lazima ushiriki moja kwa moja katika mabadiliko. Kubaliana tu na ukweli kwamba mambo yanabadilika. It is what it it is.It was what it was.It will be what it will be.Don’t stress it.
  1. Panga Ratiba Zako Vizuri– Miongoni mwa mambo ambayo husababisha stress ni pamoja na kutopangilia muda au ratiba vizuri. Kwa mfano unapojishtukia asubuhi umechelewa kuamka, ni wazi kwamba moyo wa wasiwasi huanza kukuenda mbio. Una-panic. Matokeo yake ni kwamba mambo mengine mengi yatakwenda kombo. Chukua dakika 10 au 15 usiku kuandaa kesho.
Kwa mfano, chagua nguo utakazovaa usiku. Weka kila kitu unachotakiwa kutoka nacho kesho kwenye aidha pochi au begi lako. Kama huwezi, na kuna kitu unataka kukumbuka asubuhi, jitumie ujumbe mfupi wa maneno (text) kwenye simu yako. Ukiamka bila shaka utachukua simu yako. Itakukumbusha.
  1. Kuwa Makini Katika Kuchagua Marafiki– aina ya marafiki waliokuzunguka wanaweza kuwa chanzo cha furaha au karaha. Wanaweza kuwa chanzo cha msongo wa mawazo. Chagua aina ya marafiki ambao watakusaidia kusonga mbele. Rafiki anayekukatisha tamaa kila siku,sio rafiki. Achana naye. Rafiki asiyekupa issues za maendeleo ni “adui”.Muepuke. The people in your life should be a source of reducing stress not causing more of it.
  1. Jicheke wewe mwenyewe-Kumbuka kujicheka wewe mwenyewe hususani pale unapofanya makosa. Badala ya kujipiga kichwa Ukutani au kujipiga kwenzi, jitizame kwenye kioo ujicheke. Jikumbushe kwamba wewe ni binadamu usiye kamili. Unakosea.
  1. Usiseme NDIO kwa kila kitu au kila jambo– Baadhi yetu huwa hatupendi kuonekana “wabaya”. Tunajaribu kumridhisha kila mtu. Unasema NDIO kwa kila ombi au jambo. Matokeo yake unatingwa na mambo mengi kwa mpigo ambayo kibinadamu huwezi kuyatimiza yote. Usikubali kila kitu. Wala usijisikie vibaya kusema HAPANA.
  1. Chukua Maamuzi– miongoni mwa mambo ambayo hutuacha hoi kwa msongo wa mawazo ni tabia ya kutochukua maamuzi. Maamuzi ni dawa ya kwanza ya kuondoa msongo wa mawazo. Chukua maamuzi. Unaweza ukachukua maamuzi yasiyo sahihi. Ikitokea hivyo,yatizame upya maamuzi yako na kisha fanya marekebisho. Usiogope kuchukua maamuzi. Wewe ni mkurugenzi mkuu wa maisha yako ukiachana na Muumba. Yaendeshe maisha unavyotaka wewe.
  1. Tumia Msongo Wa Mawazo Kama Mwalimu/Funzo– Kuna msemo unasema ukipewa malimau, tengeneza juisi ya malimao(make lemonade out of lemons). Unapopatwa na jambo au mambo yanayokupa msongo wa mawazo,chukua muda, tafakari. Jiulize jinsi ambavyo unaweza kutumia uzoefu ulioupata kurekebisha mambo.
  1. Ukikosea, Kuwa Mwepesi Wa Kuomba Msamaha– Miongoni mwa mambo ambayo huzidisha msongo wa mawazo ni kutokuwa mwepesi katika kuomba msamaha pale unapokosea. Wakati mwingine hata pale ambapo unaona hujakosea lakini mwenzako anaona umemkosea, omba tu msamaha yaishe. Hupungukiwi kitu. Usipokubali kujishusha na kuomba msamaha matokeo yake ni kwamba unatumia muda mwingi ukijipa moyo kwamba hujakosea. Unawaza mambo lukuki yasiyo na msingi. Kuomba msamaha kunakupa nguvu. Hutoonekana dhaifu kwa kuomba msamaha.
  1. Punguza tabia ya kulaumu wengine– Sio kila jambo linalotokea ni kwa sababu ya wengine. Wakati mwingine (na hata mwingi) ni wewe mwenyewe. Kubali kwamba unaweza kukosea. Usimlaumu mtu na kila mtu. Rekebisha kilichokwenda kombo. Life is tough my darling but so are you-Stephanie Bennet Henry
  1. Andika chini mambo 10 Ambayo unashukuru kuwa nayo– Kila mtu ana jambo ambalo analo na ambalo mtu au watu wengine hawana. Yawezekana huna hela leo lakini una afya nzuri na salama. Unaweza kuwa huna watoto lakini unao ndugu,jamaa na marafiki wanaokupenda na kukujali. Tizama mambo yaliyokuzunguka. Chagua yale ambayo yanakupendeza. Yazingatie hayo zaidi. Take a deep breath. It’s just a bad day,not a bad life.
  1. Sikiliza Muziki– Tafiti nyingi zinaonyesha kwamba muziki husaidia kupunguza msongo wa mawazo. Muziki unaweza kupunguza mhemko. Chagua muziki unaoupenda. Sikiliza. Cheza. Imba pamoja na mwimbaji. Mitandao kama YouTube ina michanganyiko chungu mbovu ya muziki. Andika tu Dance Music Mix,Feeling Happy Music, Workout Music nk utapata kila aina ya muziki. Hapa naweza kuongeza angalia filamu au shoo za televisheni za kuchekesha. Kicheko ni dawa ya mambo mengi sana. Have a good laugh. Laugh again and again.
  1. Fanya Mazoezi– Mazoezi husaidia kwa mengi. Ukifanya mazoezi unachangamsha mwili na mzunguko mzima wa damu. Ninaposema mazoezi yanaweza kuwa kitu kidogo tu kama kutembea au kunyanyua na kushusha mikono,miguu nk. Pia mazoezi yanaweza kukusaidia kuona mambo mengine ambayo huyaoni. Kwa mfano,jioni toka nyumbani kwako, tembea mtaani. Onana na majirani zako.Wasalimie na wao wakusalimie. Furahia uumbaji wa Mwenyezi Mungu wa dunia. Furahia mandhari unayoiona.


  1. Mpigie simu rafiki yako wa zamani– Kila mtu anaye rafiki ambaye mmeshibana. Unaye rafiki ambaye mmepitia mambo mengi pamoja. Mazuri na mabaya. Mpigie simu kisha mkumbushane yale mazuri na ya kufurahisha mliyopitia. Chekeni kwa pamoja. Mimi ninalo kundi la marafiki tuliosoma pamoja sekondari pale Umbwe. Huwa tunakutana kwa WhatsApp na kukumbuka mambo mengi tuliyopitia. Tunacheka.
  1. Soma Kitabu– Hii ni mojawapo ya mbinu ambazo mimi binafsi huzitumia sana pindi mambo yanapokuwa magumu. Huchukua kitabu kizuri cha hadithi(novel) na kujizikia humo nikisoma. Waandishi ninaowapenda zaidi ni kama Lee Child, John Grisham, J.D Robb, James Patterson, Tom Clancy na David Baldacci.
  1. Pata Usingizi Wa Kutosha– Binadamu wa kawaida anatakiwa kupata muda wa masaa 6 mpaka 8 ya kupumzika(kulala). Kinyume chake, unakuwa unajiandaa kwa hatari za kiafya na pia msongo wa mawazo. Mtu ambaye hajapumzika vizuri ni mwepesi wa kughafilika. Atahamaki hata kwa mambo madogo tu. Hamaki huzusha mikasa na hugombanisha watu. Athari za kutopata usingizi wa kutosha na mbinu za kufanya ili kulala(hususani unaposhindwa kulala kutokana na mawazo nk) nitaziongelea siku moja.
  1. Chagua Kuwa Mwenye Furaha– Muumba ametupa uwezo wa mambo mengi sana. Mojawapo ni uwezo wa kuamua yale tunayoyataka na yale tusiyoyataka. Uamuzi ni wako. Jipe moyo na kuamua kuwa mwenye furaha. Jiepushe na hali au mazingira ambayo yatakukosesha amani na furaha. It all begins and ends in your mind. What you give power to has the power over you if you allow it.
Je, ni mbinu gani ambazo unazitumia zaidi pindi unapokuwa na msongo wa mawazo(stress) au unapohisi furaha na amani imeota mbawa? Niandikie. Usisahau kumtumia ndugu,jamaa na marafiki.Unaweza kuokoa maisha ya mtu.

#MACHAS OFFICIAL SITE

No comments:

Post a Comment