Monday, November 28, 2016

SERIKALI YATANGAZA KIAMA KWA WALIOGHUSHI VYETI>>>>

Kiama cha walioghushi vyeti ama kutumia vyeti vya watu wengine kwa lengo la kujitafutia ajira serikalini, kinakaribia baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), kubainisha kuwa liko katika hatua za mwisho za kukamilisha uhakiki wa vyeti vya watumishi hao.
Akizungumza na gazeti la Habarileo kwa simu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi, alisema mpaka sasa maofisa wa baraza hilo waliosambazwa mikoani kufanya uhakiki huo, wengi wao wamerejea na wachache waliobaki wanakamilisha kazi hiyo ili warejee Dar es Salaam.
“Ni kama mchakato wa uhakiki uko katika hatua za mwisho na kinachofanyika sasa ni kufanya majumuisho,siwezi kusema ni lini hasa tutamaliza lakini kazi kubwa tumemaliza kinachofanyika ni majumuisho,” alisema Nchimbi.
“Sisi tunafanya uchambuzi wa vyeti hivi tulivyoletewa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuvihakiki, baada ya hapo tutatoa mrejesho kwa taasisi husika kuwa kati ya vyeti ilivyotuletea vingapi ni vya kughushi na taasisi hiyo ndio itakayochukua hatua,” aliongeza.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa Necta, mtu akifanya udanganyifu wa vyeti kwa kughushi au kutumia cheti kimoja kwa watu wawili, baraza hilo lina mamlaka ya kuwashtaki wahusika ikiwa ni pamoja na kumnyang’anya cheti mwenye cheti.
Hivi karibuni, serikali ilitangaza rasmi kuanza kampeni ya kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wote walioajiriwa katika sekta hiyo wakitumia vyeti bandia.
Kutokana na kuanza kampeni hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano iliwataka watumishi hao waanze kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya kufikiwa na mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi wa umma yanayokuja nchini.
Tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki ameiagiza Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu (Utumishi) kuwachukulia hatua stahiki watumishi watakaobainika kutumia vyeti visivyo vyao ili kupata ajira serikalini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano ya mwaka 2004, ni kosa la jinai kughushi vyeti.

No comments:

Post a Comment