SHIRIKA la Fedha la Kimataifa (IMF) limetoa ripoti kuhusu mustakabali wa uchumi wa dunia, likibatilisha makadirio ya awali lililotoa Januari mwaka huu kuhusu mwelekeo wa ukuaji wake.
Awali, mapema mwaka huu, IMF ilisema uchumi wa dunia utakua kwa asilimia 3.4 mwaka huu na asilimia 3.6 mwaka ujao.
Lakini kwa mujibu wa ubashiri wake mpya uchumi huo utakua kwa asilimia 3.2 mwaka huu na asilimia 3.5 mwaka 2017 likitahadharisha kuwa unakabiliwa na hatari ya kutoongezeka.
Licha ya hilo, IMF imepandisha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa China kwa mwaka huu na mwakani hadi asilimia 6.5 na asilimia 6.2.
Baada ya mashirika maarufu ya Marekani ya kutathmini uwezo wa nchi kuhimili madeni ya Moody’s na Standard & Poor’s kushusha hadhi ya China kwenye tathmini zao, ripoti hiyo mpya inatarajia kuongeza imani ya watu na mustakabali wa ukuaji wa uchumi wa China.
Mchumi Mkuu wa IMF, Maurice Obstfeld, anasema uchumi wa dunia unaendelea kufufuka, lakini kasi yake ni ya taratibu mno na inasikitisha watu na kwamba itasababisha ukuaji wake kukabiliwa na hatari nyingi zaidi.
Ukuaji taratibu wa uchumi wa dunia umedumu kwa muda mrefu sasa.
Kwa mujibu wa makadirio mapya kuhusu mustakabali wa uchumi wa dunia, ikilinganishwa na hali ya mwaka 2015, ongezeko la uchumi huo kwa mwaka huu litakuwa ni asilimia 3.2 tu, na mwakani litafikia asilimia 3.5.
Obstfeld alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne wiki mbili zilizopita mjini Washington, Marekani, ambapo ripoti kuhusu mustakabali wa uchumi wa dunia ilitolewa hadharani.
Kwenye hotuba yake, Obstfel alitoa tahadhari kuhusu ufufukaji wa taratibu na udhaifu wa uchumi wa dunia na kusema kupungua kwa ongezeko la uchumi kunaweza kupunguza thamani ya sarafu duniani, kuchochea utaifa na kusababisha migogoro ya siasa za kijiografia.
Ripoti hiyo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa IMF wa kufanya mkutano na wanahabari mara mbili katika nusu ya kwanza na ya pili ya mwaka.
Hiyo ni mbali ya mkutano wa majira ya kuchipua na ule wa majira ya kupukutika ili kutangaza ripoti kuhusu mustakabali wa uchumi wa dunia, na pia kurekebisha ripoti hiyo katikati ya mwaka huo na mwanzoni mwa mwaka unaofuata.
Ripoti hiyo inayoitwa ‘polepole na muda mrefu’, imeonesha wazi kuwa uchumi wa dunia umeongezeka taratibu kwa muda mrefu.
Ukuaji wa aina hiyo una athari mbaya, kupunguza uwezo wa uzalishaji, hivyo kuathiri matumizi na uwekezaji.
Kutokana na hilo, IMF imetoa wito kwa mataifa mbalimbali kuchukua hatua kuchochea uchumi kama vile kuhimiza mageuzi ya kimuundo, kutoa sera za uchochezi wa kifedha na kuongeza utoaji wa sarafu sokoni.
Kuhusu ongezeko la uchumi wa China hadi asilimia 6.5 kwa mwaka huu na asilimia 6.2 mwakani kinyume na ilivyodhaniwa awali Obstfel anasema:
“Kupandisha makadirio kuhusu ukuaji wa uchumi wa China kunaonesha imani kwa hatua na sera nyumbufu zilizotangazwa na Serikali ya China zinazolenga kukuza uchumi wake, na inaaminika kuwa uchumi wa China kwa mwaka huu unaweza kuongezeka kwa asilimia 6.5.”
Ripoti hiyo inaona kuwa China inashuhudia mchakato wa mageuzi ulio muhimu lakini wenye utata, na inatarajia kutafuta maendeleo endelevu ya uchumi yanayopatikana kwa matumizi na huduma.
Anasema mwishoni, mchakato huo utainufaisha China pamoja na dunia nzima.
IMF pia imesema uchumi wa nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara unakadiriwa kukua kwa asilima tatu kwa mwaka huu, kiasi ambacho kimepungua kutoka asilimia 3.4 ya mwaka jana na asilimia 5.1 ya mwaka juzi.
Nchi mbili za Nigeria na Afrika Kusini zinazoongoza kiuchumi Kusini mwa Sahara Afrika, ambazo zimechangia nusu ya pato la kanda hiyo, zilionekana kuathiri ongezeko la kikanda mwaka jana.
Kwa mujibu wa takwimu za IMF, ukuaji wa Nigeria, nchi inayouza nje mafuta kwa wingi zaidi katika kanda hiyo, ulipungua hadi asilimia 2.7 mwaka jana kutoka asilimia 6.3 ya mwaka 2014.
Aidha Afrika Kusini, nchi inayouza nje madini kwa wingi zaidi katika kanda hiyo ilishuhudia ongezeko la asilimia 1.3 mwaka jana kutoka asilimia 1.5 ya mwaka juzi.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa msukosuko wa wakimbizi wa Syria, wasiwasi na ugaidi, upigaji kura za maoni utakaofanyika Juni mwaka huu kuamua iwapo Uingereza ijitoe au ibaki Umoja wa Ulaya (EU).
Hali kadhalika, vizuizi vya ukuaji vya masoko mapya yaliyoibuka, kupungua kwa nguvu za ongezeko la makundi ya kiuchumi yaliyoendelea, kuyumbayumba kwa bei za bidhaa zinazoagizwa kwa wingi, na mvua kubwa za El Nino, vyote vitaongeza hali ya kutokuwa na utulivu kwa ufufukaji wa uchumi wa dunia.
Kama hayo hayatoshi, iwapo matokeo ya kura za maoni yataifanya Uingereza kujitoa EU hilo litakuwa pigo kubwa kwa uchumi wa dunia, ambao tayari u dhaifu.
Shirika la Habari la Uingereza Reuters linaona kuwa hili ni onyo kali zaidi kuwahi kutolewa na IMF kuhusu hatari ya Uingereza kujitoa EU.
Obstfel amesisitiza kuwa hivi sasa ufufukaji wa uchumi wa dunia ni dhaifu na kuna uwezekano wa kupungua, hivyo ni lazima kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto hizo.
“Narudia kwa mara nyingine tena kuwa ufufukaji wa taratibu wa uchumi umewafanya watunga sera wasiwe na nafasi nyingi za kufanya makosa,”
“Na kama watunga sera wa nchi mbalimbali wakitambua ipasavyo hatari zinazowakabili kwa pamoja na kuchukua hatua zenye uratibu, itaweza kuongeza imani ya watu, kuhimiza ukuaji na kulinda vizuri mchakato wa kufufuka kwa uchumi wa dunia,” anasema.
No comments:
Post a Comment