Monday, January 2, 2017

HIKI NDICHO KILICHOMPONZA ALIYEKUWA BOSI WA TANESCO,NDUGU MRAMBA KUIPOTEZA NAFASI NA KAZI YAKE HIYO>>>>

FELICHESMI MRAMBA,ALIYEKUWA MANAGING DIRECTOR WA TANESCO
 
STORY BY JULIE KAVISHE-JOURNALIST MACHAS BLOG
Hatua ya Shirika la Umeme ya kupandisha bei ya umeme bila kushirikisha mamlaka nyingine za Serikali, zimemgharimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Felchesmi Mramba, ambaye Jumapili hii amefutwa kazi na Rais John Magufuli.
Kabla ya kutengua uteuzi wa Mramba, Rais Magufuli ambaye Jumapili hii alisali mjini Bukoba katika kanisa la Bikira Maria, Mama mwenye Huruma la mjini Bukoba, alisema Tanesco haikumshirikisha yeye, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Ewura juzi ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 baada ya Tanesco kuomba gharama zipande kwa asilimia 18.19, lakini hatua hiyo ilisitishwa na Profesa Muhongo.
“Waliopandisha umeme hawakuja kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi, hawakuuliza hata waziri mwenye dhamana, ya nishati hawakumuuliza hata Makamu wa Rais, Waziri Mkuu haiwezekani mtu akae peke yake na afanye maamuzi yake pekee bila kushirikisha mamlaka nyingine,” alisema Rais.
Ateua bosi mpya, taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli baada ya kutengua uteuzi wa Mramba, amemteua Dk Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.
Mwinuka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na hadi uteuzi wa jana, alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa Viwanda Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akiwa kanisani, Rais Magufuli alimpongeza Profesa Muhongo kwa hatua ya kusimamisha kupanda kwa bei ya umeme. “Namshukuru waziri wa nishati kwamba ameshatengua maamuzi hayo, kwa hiyo umeme hakuna kupanda”.
Rais Magufuli alisema haiwezekani watu mnapanga mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika mikakati hii mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme hadi vijijini na umeme huo unaenda hadi kwa watu maskini walioumbwa kwa mfano wa Mungu, halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo chake anakwenda kusimama kupandisha bei ya umeme.
Akionekana kukereka kwa hatua hiyo ya kupandishwa kwa bei ya umeme, Rais Magufuli alisema, “Na ndio maana baba askofu nalizungumza hili kwamba majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua, ndio maana naomba sana Watanzania muendelee kutuombea, lengo la serikali ninayoiongoza ni kwenda na wananchi wa kipato cha chini.”
 
CHANZO CHA TAARIFA: HABARI LEO
 

No comments:

Post a Comment