Watu wanaoishi karibu na barabara kuu huwa wana viwango vya juu vya matatizo ya kiakili, ambayo kwa Ujumla hufahamika kama Dementia.
Watu wenye dementia hukabiliwa na matatizo ya kukumbuka mambo pamoja na uwezo wao wa kutumia ubongo kwa jumla.Hisia zao hubadilika pia na kwa muda mrefu wamekuwa wakidhaniwa kuwa wenye wazimu au watu wenye kichaa.
Matokeo ya utafiti ambayo yamechapishwa katika jarida la Lancet yanaonyesha asilimia 11 ya visa vya dementia ambavyo hutokea katika eneo la hadi mita 50 kutoka kwenye barabara huenda vinatokana na magari.
Watafiti, ambao waliwachunguza watu karibu milioni mbili nchini Canada kwa kipindi cha miaka 11 wanasema uchafuzi wa hewa na kelele kutokana na magari huenda vinachangia katika kuathiri ubongo wa wakazi.
Wataalamu wa dementia nchini Uingereza wanasema matokeo ya utafiti huo yana uzito lakini yanahitaji kuchunguzwa zaidi.
Inakadiriwa kwamba watu karibu milioni 50 kote duniani wanatatizwa na ugonjwa wa dementia.
Hata hivyo, chanzo hasa cha ugonjwa huo hakijabainika.
Utafiti huo uliofanywa katika mkoa wa Ontario nchini Canada kati ya 2001 na 2012 uligundua watu 243,611 wenye matatizo hayo ya kiakili.
Visa viliongezeka miongoni mwa walioishi karibu na barabara kuu.
Wakilinganishwa na waliokaa zaidi ya mita 300 kutoka kwa barabara kuu, hatari ya kuugua ugonjwa huo ilikuwa:
- 7% zaidi kwa waliokuwa 50m
- 4% zaidi kati ya 50-100m
- 2% zaidi kati ya 101-200m
hata hivyo Watafiti walizingatia mambo mengine ambayo huenda yakachangia ugonjwa huo yakiwemo umaskini, unene, viwango vya elimu na uvutaji wa sigara kuhakikisha havikuathiri matokeo.
Dkt Hong Chen kutoka Ontario, ambaye ni mmoja wa watafiti waliohusika, anasema ikizingatiwa kwamba watu wengi wamekuwa wakihamia mijini na barabara na magari kuongezeka, kuna haja ya uchunguzi zaidi kuhusu athari za magari na barabara kama vile uchafuzi wa hewa na kelele.
Watafiti hao wanadokeza kwamba kelele, vumbi, chembe za naitrojeni oksaidi na chembe za mipira kutoka kwa tairi za magari huenda vinachangia kuongezeka kwa ugonjwa wa dementia kwa wanaoishi karibu na barabara kuu.
Hata hivyo, utafiti huo uliongozwa sana na maeneo ambayo watu wenye dementia wanaishi.
Hauwezi kuthibitisha kwamba barabara ndizo zinazosababisha ugonjwa huo...
No comments:
Post a Comment