Monday, July 4, 2016

TAMKO LA UVCCM KUHUSIANA NA BAVICHA KWA KILE KINACHOTARAJIA KUFANYIKA DODOMA

UMOJA WA VIJANA, CHAMA CHA MAPINDUZI
 
 
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamda Shaka
 
Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) umeingia katika mvutano mkubwa na Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) kuhusu Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho tawala uliopangwa kufanyika Julai 23 mwaka huu mjini Dodoma.

UVCCM wameionya BAVICHA kuhusu mpango wao wa kutaka kukusanyika mjini Dodoma siku hiyo kwa lengo la kuzuia mkutano huo kwa madai kuwa unakiuka amri halali ya polisi ya kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano yote ya kisiasa nchini.

Onyo hiyo limetolewa na  Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamda Shaka ambaye aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa watawakabili kwa nguvu zote BAVICHA endapo wataamua kuendesha siasa zinazolenga kuvuruga amani na kuleta hofu katika jamii na kutishia maisha.

Alisema umoja huo hautaona shaka kutumia mbinu zilizotumiwa na wapiganaji wa Maumau miongo kadhaa iliyopita nchini Kenya.

“Hatutaona muhali kupita njia zilizotumiwa na wapiganaji wa Maumau wa Kenya ili kukihami chama, kulinda viongozi wake na kupigania hadhi na heshima yetu,” alisema Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM.

CCM inatarajia kufanya mkutano mkuu maalum Julai 23 mwaka huu ambapo Rais John Magufuli atakabidhiwa rasmi uenyekiti wa chama hicho kutoka kwa mtangulizi wake, Dk. Jakaya Kikwete.
 
$MACHAS OFFICIAL SITE

No comments:

Post a Comment